Baba ni jina au cheo ambacho kimetokana na neno “Abba” yaani “mwanzilishi /chanzo”. Ndiyo maana mwanzilishi wa maisha yetu hapa duniani tunamuita Baba yetu wa mbinguni. Utagundua hata waanzili shi wa nchi au taifa wanaitwa “Baba wa Taifa.”
Kwa hiyo nafasi ya ubaba kwako ni nafasi inayomaanisha kwamba wewe ni mwanzilishi. Wakristo tunamuita Ibrahimu Baba yetu wa imani kwa sababu imani yetu ilianza kufunuliwa kuanzia kwake. Wenye watoto wanaitwa Baba wa watoto kwa sababu wao ndiyo wamewaanzisha hao watoto.
Baba ni mbegu. Mbegu ndani yake kuna mwanzo wa mmea au kitu fulani. Kuwa Baba ni zaidi ya kuwa na watoto uliowazaa. Kuwa Baba kuna maana pana sana ambayo tutaingia kwa undani kwenye kipengele kinachofuata. Lakini, tambua kwamba mwanaume yeyote anawajibu wa kuwa Baba hata kama hana watoto aliowazaa kibaiolojia. Maadamu Baba ni mwanzilishi au chanzo, basi kila mwanaume amepewa jukumu la kuwa mwanzilishi au chanzo.
Ijapokuwa mwanaume anatarajiwa kuwa baba, hiyo haimaanishi kwamba moja kwa moja anakuwa ni baba eti kwa sababu ni mwanaume. Kuna gharama lazima anapaswa kuzilipa ili kustahili kuitwa baba. Sasa, kama upo kwenye mahusiano kama mwanaume na unatarajia siku moja uwe baba kw watoto wako unapaswa kujua hilo zoezi la kuwa baba linapaswa kuanza sasa hivi. Leo hii.
Kwa Nini Mwanaume Anatakiwa Kulipa Gharama ya Kuwa Baba?
(a)Kwa Sababu Mungu Huzungumza na Kutoa Maelekezo kwa Baba Kuhusu Vizazi. (1Yohana2:13)
“Nawaandikia ninyi ,akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo…”
Mungu anapotaka kutoa ujumbe kwa vizazi vilivyopo na vijavyo huwa anazungumza na baba. Huwa anatoa maelekezo kwa akina baba. Huwa anamwaga siri zake na kuwaambia akina baba. Huwa ana waamini akina baba kwa jukumu la kukomboa vizazi. Mungu hafanyi maagano ya vizazi na mtu yeyote tu ilimradi ni mtu. Bali Mungu hufanya maagano na akina baba. (Kumbukumbu 8:18)
“Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”
Mungu hapa anakumbusha wajibu wa wana wa Israeli kwamba wanapaswa kumkumbuka BWANA, Mungu wao ili lile agano alilolifanya Mungu pamoja na baba zao alifanye imara. Tayari tunaona kulikuwa na agano kati ya baba zao wana wa Israeli na Mungu. Hili agano lilikuwa linawagusa wana wa Israeli lakini wati a saini wa hili agano hawakuwa wana wa Israeli wote bali walikuwa Mungu pamoja na baba zao wana wa Israeli.
Tunaanza kuona agano la kwanza kabisa kuhusu vizazi ni agano la Mungu na baba yetu wa Imani, Ibrahimu (Mwanzo17:1-25). Pia agano la Mungu na Isaka (Mwanzo 26). Pia agano la Mungu na Yakobo (Mwanzo32). Lakini ona Mungu anavyojitambulisha kwa vizazi. Huwa anajitambulisha kupitia baba. Alijitambulisha kwa kizazi cha wana wa Israeli kupitia baba zao (Kutoka3:6). “Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo…”
Vilevile, Mungu alitoa maelekezo ya urithi wa imani kwa kizazi kijacho cha wana wa Israeli kupitia baba zao. (Yoshua 4:21-22) “Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini? Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu. Kwa sababu BWANA, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hata mlipokwisha kuvuka kama BWANA, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka;”
Ni lazima mwanaume utambue kwamba mbele za Mungu una nafasi ya ubaba hapa duniani na Yeye anakutegemea utambue na ukae kwenye hiyo nafasi ili utumike kumtambulisha kwa vizazi vijavyo. Hilo ndilo jukumu lako la kwanza kama mwanaume hapa duniani. Usipojua nafasi yako vizuri na ukaanza kutumika basi utashangaa shetani anaitumia nafasi yako kwa kukutumia wewe ili kusababisha maangamizo kwa vizazi vyako vya sasa na baadaye.
(b)Baba ni CHANZO. Hivyo, Uzao Wako na Watu wa Nyumba Yako Watakuomba Mahitaji Wakikutarajia Ukidhi Mahitaji Yao. (Yohana1:1-5, 16)
“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, name ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu name ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. … Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; name nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”
Yesu anaeleza uhusiano uliopo kati yetu na Mungu. Kwamba Yeye Kristo ni mzabibu. Baba Yake (ambaye ni Baba yetu pia) ni mkulima. Na sisi ni matawi. Haipingiki kwamba ukiona zao limemea ujue kuna mkulima aliyepanda mbegu (chanzo). Hivyo, Baba anayezungumzwa na Yesu kuwa ni mkulima, ndiye mwanzilishi wa mzabibu huo maana ndiye aliyekuwa na mbegu akapanda na kutoa mzabibu.
Ukisogea kusoma Yohana15:16 utagundua kwamba Baba ndiye anategemewa kuombwa mahitaji yote. Kama baba ndiye ana jukumu la kuombwa mahitaji ujue vilevile ana jukumu la kuhakiki sha anahudumia kwa kutoa vyote anavyoombwa. Mwanaume ambaye hatalipa gharama hii hatojua kuwa nafasi ya kuhudumia familia yake, mke, watoto wake pamoja na jamii ni jukumu lake.
Ndiyo maana wapo wanaume wajinga wasiojua kweli hii wanaoona mzigo kutoa matumizi ya familia na kuhudumia watu wa nyumba yake. Wengine wanazikimbia na kuzitelekeza familia zao kwa sababu hawajajifunza kulipa gharama hii ya kuwa chanzo. Wengine wanaacha jukumu la kuleta chakula nyumbani na kuhudumia mahitaji ya familia kwa akina mama. Wanawaachia wake zao walete chakula nyumbani huku wao hawajishughulishi kwa lolote.
Ni kweli, inawezekana kuna nyakati Mungu hupitisha baraka kwa mke. Na yeye anaweza kufanya kwa sehemu kubwa kuhusu kuhudumia gharama za kifamilia. Hata hivyo, kama baba unapaswa kuwa chanzo cha kuongoza namna rasilimali hizo zitumike na namna ziweze kuongezeka. Usiwe mtu wa kukaa bia kufanya lolote la kujenga.
Huu ni uovu wa kiwango cha juu sana. Mwanaume wewe ni chanzo. Wewe ni kama chemichemi. Unatakiwa kukidhi kila mahitaji mema jema kwako mwenyewe, kwenye Ufalme wa Mungu, na kwenye familia yako. Kwa maana kila kutoa kuliko kwema, hutoka kwa Baba wa mianga. Na huyo Baba wa manga anakutarajia uwe na tabia ya kutoa kama Yeye alivyo.
(c) Mungu Anaheshimu na Kusikiliza Mamlaka ya baba (Mwanzo 31:19-35 na Mwanzo 35:16-18)
“Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akavii ba vinyago vya babaye. Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia. Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi. Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia, akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi. Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi. Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka walio twaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwafuraha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.
Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu? Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang’anya binti zako kwa nguvu. Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli ameiiba.
Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka kati ka hema ya Lea, akaingia katika hema ya Raheli. Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona. Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago…”
Nini kinatokea baadaye kwa sababu ya matamko ya Yakobo? Soma Mwanzo 35:16-18
“Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito. Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini.”
Kwa nini Mungu ana heshima na kusikiliza mamlaka ya baba? Ni kwa sababu yeye mwenyewe ndiye liyekasimisha mamlaka hayo kwa mwanaume kuwa baba hapa duniani. Na Mungu ni mwadilifu maana hawezi kupinga na neno lake mwenyewe. Ndiyo maana Adamu alipowapa mimea na wanyama majina, Mungu aliheshimu na hakupinga. Ndivyo ilivyokuwa. Alichokiamuru Adamu ndicho kilichofanyika.
Yakobo aligundua kanuni hii na ndiyo maana mkewe alipompa mtoto wao jina Benoni likimaanisha uchungu maana mkewe alipata uchungu mkali na baada tu ya kujifungua alifariki.
Yakobo anabadili jina na kumwita Benyamini. Ikawa hivyo. Mtoto akaitwa Benyamini na siyo Benoni kama alivyotaka mama yake.
Hata hivyo, kufa kwa mke wake Yakobo kulisababishwa na nadhiri aliyoiweka Yakobo mwenyewe kwa kutokujua kwamba itampata mkewe. Yakobo alitamka atakayepatikana na miungu ya baba mkwe wake na afe. Bila kujua mkewe ndiye aliyekuwa ameificha miungu hiyo.
Tambua vyovyote utakavyoamua kuhusu wewe au watu wanaoitwa kwa jina lako ndivyo itakavyokuwa kwako na kwao. Mungu anaheshimu maamuzi hayo. Ukiwa na ufahamu huu itakusaidia kutumia mamlaka yako kusababisha baraka na mafanikio kwenye kizazi chako lakini usipofahamu vizuri unaweza kushangaa umetamkaa na kuamua kivyovyote ambavyo huenda maamuzi hayo yakagharimu vibaya kizazi chako sasa na baadaye.
Nimeandika kitabu ambacho kimelenga kuwasaidia wanaume na wanawake wanaojiandaa kuingia kwenye mahusiano yatakayowapelekea kuingia kwenye ndoa. Kinaitwa GHARAMA ZA KULIPA KUONGEZA THAMANI YA MAHUSIANO YAKO. Unapaswa kukisoma kikusaidie wewe na mwenza wako mtarajiwa. Kukipata unaweza kuwasiliana na mwandishi kwa namba za simu 0657342567.
Nakutakia matokeo chanya.
Leave a comment