Mathayo 6:33 (SUV): Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
Mungu ni Mungu wa mpangilio, na katika mpangilio Wake, kusudi huja kabla ya mahitaji mengine. Watu wengi hukimbilia “vitu” pesa, hadhi, au fursa wakitumaini kuwa vitawaletea utoshelevu. Lakini hekima ya ufalme ni tofauti “Tafuta kwanza Ufalme wake na haki yake”
Kutafuta Ufalme wa Mungu ni kuishi kusudi la Mungu, kumfuata Yeye na haki Yake kuliko vyote. Sio kupuuza mahitaji ya kila siku, bali ni kuelewa kuwa unapoweka ajenda ya Mungu mbele, kila kitu kingine huja kama Mungu alivyo kusudia.
Mafanikio ya kweli hayapatikani kwa kuangalia ni kiasi gani nilicho pata, bali kwa kiwango gani nimeweza kuwa karibu na kusudi la mbingu hapa duniani. Tunapoelekeza macho yetu kwenye kusudi la Mungu ndio njia rahisi ya kuyapa maisha yetu maana na thamani. Tutaanza kunena kwa hekima, maneno yetu yatajaa neema, tutaathiri maisha ya kizazi kinacho kuja baada yetu.
Usifanye kosa la kuanza kutafuta kwanza nyongeza kabla ya lili lililo kuu Ufalme wa Mbinguni. Mungu habariki walio upotevuni hubariki walio katika kusudi lake/mpangilio wa vipaumbele vyake ambayo ni Ufalme wake.
Shallom!
SOMO LA ZIADA: Methali 19:21; Warumi 12:2
TONO LA DHAHABU:
” Ufalme unapokuwa kipaumbele chako, mbingu huyafanya maisha yako kuwa kipaumbele chake. Kusudi ni sumaku ya kuvuta vyote unavyo viitaji kutoka kwa Mungu.“
OMBI:
Baba, nakushukuru kwa kunikumbusha kutafuta kwanza Ufalme Wako. Naweka chini kila tamaa isiyoambatana na kusudi lako juu ya maisha yangu. Nisaidie niishi kila siku nikilifuata moyo Wako. Ninaamini kuwa nikifanya hivyo, kila ninachohitaji kitaongezwa, kwa jina la Yesu, Amina.
Leave a comment