Ushahidi Kwamba Wewe ni Kiumbe wa ajabu Kuliko Maajabu Saba ya Dunia
“Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani, Misingi yote ya nchi imetikisika. Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye Juu, enyi nyote.”
Wengi kwa kujua wao ni binadamu tu, wamekuwa wakiishi kwa kuridhika, hawatarajii wala kujifikiria zaidi ya hapo, wamejiwekea mipaka kwenye maeneo mengi ya maisha yao ya kiroho na kimwili.
Kwa hivyo, wanatembea gizani – ambapo kuna mambo yanatokea kwenye maisha yao bila wao kujua, kuna uharibifu unafanyika bila wao kujua, kuna kudumaa kunafanyika bila wao kujua; kuna hazina ya utajiri kwa ajili yao lakini hawaioni; na hii yote ni kwa sababu hawajui wala hawana ufahamu kuhusu wao ni akina nani.
Mungu akiwatazama anawaona wao ni miungu, wana wa Aliye Juu, nyote; ya kwamba kuna mambo wanapaswa kuyaamuru yatokee kwa mamlaka ya kujua wao ni miungu tena wana wa Aliye Juu.
Kuna mambo wanapaswa kuyaamua kwa mamlaka ya utambulisho wao kama wana wa Mungu. Kuna uovu walipaswa kuukemea na kuung’oa na kuubomoa kwa mamlaka ya utambulisho wao kama wana wa Mungu.
Mungu hawatazami kama watu tu; bali anawaangalia kama miungu, wana wake Yeye Aliye Juu.
Na kuazia leo unapaswa kujua kuwa wewe ni zaidi ya kuwa mwanadamu tu; mwana aliyezaliwa na mzee fulani maarufu, au tajiri, au fukara bali wewe ni mungu, mwana uliyezaliwa na Mungu, aliye juu.
Inawezekana unajiona hustahili kuitwa mwana wa Mungu Aliye Juu kwa sababu umezaliwa na wazazi ambao ni waganga wa kienyeji au wachawi. Hii haiondoi ukweli kwamba, machoni mwa Mungu, wewe ni wake.
Adui anatumia hila kupitia mawazo yako kukuzuia usiiamini hii kweli ili usije ukaanza kuitika na kutenda sawasawa na utambulisho wako halisi.
Ni kweli umezaliwa katika dhambi, na inawezekana mimba yako ilitungwa katika dhambi kama mfalme Daudi anavyosema “Tazama , nilizaliwa nikiwa na hatia; Mama yangu alinichukua mimba nikiwa na dhambi.” (Zaburi 51:5) bado unaweza kuomba rehema na kurejeshwa na BWANA na ukaanza kutembea kama mwana wa Mungu Aliye Juu
Ushahidi wa Kwanza: SURA NA MFANO WA MUNGU (Mwanzo 1:26)
“Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi.”
Kuna watu ambao wanajichukulia kawaida kwa sababu wanaona wamezaliwa na wazazi wa kawaida, ambao wana sura za kawaida; labda sio sura nzuri kama waliyotaka na ikawafanya wao kutokea na sura ambazo wao husema ni mbaya au watu wanawaambia ni sura mbaya.
Ukweli ni kwamba sura yako uliyonayo ni sura kutoka kwa Mungu mwenyewe. Vile Mungu anavyofanana ndivyo hivyo unayofanana. Wewe haufanani na baba yako au mama yako au ndugu zako tu bali unafanana na Mungu. Hili sio jambo la kulichukua kwa ukawaida.
Na hiyo taswira yako haiishii kwenye sura inayoonekana tu bali inaendelea hadi kwenye tabia na hulka. Mungu amekuumba akiwa amekusudia ufanane naye kisura na tabia pia. Uwe na tabia ya Mungu. Hili sio jambo la kulichukua kikawaida kabisa.
Pengine rafiki zako au majirani wanakufananisha na bibi yako aliyekuwa na tabia fulani mbaya; inawezekana unafananishwa na ndugu yako wa kike au wa kiume kutokana na tabia zake na hiyo inakuumiza na kukufanya ujione mtu duni na wa hali ya kawaida sana. Unapaswa kujua pia kwamba wewe ni mfano wa Mungu. Mungu anakufananisha nae. Ndivyo alivyokuumba, kwa sura na mfano wake – mpaka kwenye tabia.
“Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,”
Unapaswa kutambaa kuwa hujaumbwa kikawaida. Bali umeumbwa na njia ya ajabu halafu ya kutisha. Uumbaji wako ni ajabu, unastaajabisha – unashangaza.
Kwa hiyo unapowaambia watu kuhusu wewe ni nani kulingana na Mungu anavyokuona, usishangae wakikushangaa, kwa sababu wanapaswa kushangaa maana unashangaza.
Hupaswi kuruhusu watu wakuchukulie kawaida na wewe unawaacha tu. Unapaswa kuwaambia kwa ujasiri ya kwamba; “Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu … zitokazo kwa BWANA…” (Isaya 8:13)
Kama huwa unatamani kuona maajabu ya dunia, basi hutakiwi kuyatafuta kwenye chaneli fulani ya wanyama, au kusafiri kutizama maajabu kwenye milima kama mlima Kilimanjaro. Unapawa kujiangalia mwenyewe kwa kuwa wewe ni maajabu unayoyatafuta.
Wewe ni maajabu unayoyatamani. Wewe ni maajabu ambayo watu wanayaomba na kuyasubiria. Yaani, Mungu anajua hivyo, na shetani naye anajua hivyo. Inasikitisha sana kama wewe hutakuwa unafahamu kwamba wewe ni maajabu.
Halafu hujaishia kuwa ajabu tu. Pia, wewe ni wa kutisha; kiasi ambacho shetani anapokutazama anapaswa kuogopa, anapaswa kutetemeka, anapaswa kuwa na hofu.
Yale mambo unayoyaogopa yanapaswa kukuogopa wewe. Vile unavyoyaogopa, yenyewe yanakushangaa, halafu yanakucheka maana yenyewe yanajua ukweli ya kwamba hayo mambo ndiyo yanayopaswa kukuogopa wewe.
Wewe ni zaidi ya unavyojiona, wewe ni zaidi ya unavyojifikiria, wewe ni zaidi ya watu wanavyokuona – wewe ni kiumbe wa ajabu tena kiumbe wa kutisha.
KUNA ZAIDI YA UNAVYOJIONA NA UNAVYOONEKANA
NAMNA MBALIMBALI ZA AJABU AMBAZO MUNGU AMETUMIA KUWALETA WATU DUNIANI:
(I) Mtu Kutoka Mavumbi ya Ardhi (Mwanzo 2:7)
“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”
Ni jambo la ajabu sana kwamba, Mungu anamtengeneza mtu kwa kutumia mavumbi ya ardhi halafu akapulizia pumzi yake na mtu akawa nafsi hai.
Inaweza kudhaniwa ni jambo rahisi kutengeneza mtu kwa mavumbi ya ardhi kama mfinyanzi anavyoweza kufinyanga kinyago fulani mfano wa mtu. Lakini hapa nataka uone kwamba, Mungu hakufanya kama wafinyanzi wa kibinadamu wafanyavyo (Ijapokuwa usipokuwa makini unaweza kufananisha).
Mungu alivyomfinyanga mtu, hakutokea kinyago bali alitokea mtu ambaye ndani yake kuna viungo kama moyo, mishipa ya damu, figo, viungo ya uzazi, ubongo, uti wa mgongo, mapafu, seli za ngozi, maini, utumbo, kibofu na mifumo yote ya mwili kama vile mfumo wa upumuaji, mfumo wa kuondoa takamwili, mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, mfumo wa uzazi na kadhalika.
Hapo ndio utajua Kumbe vumbi linaweza kufanyika damu, linaweza kufanyika mishipa, linaweza kufanyika seli, linaweza kufanyika mifupo, na uroto, na ubongo, na ngozi, na maini, na mapafu, na kibofu na vyote vilivyomo ndani ya mwili wa mwanadamu.
Sasa nionyeshe mfinyanzi ambaye ameweza kufanya kama Mungu, kufnyanga mtu kwa kutumia mavumbi na kufanya viongo vyote na mifumo yake ndani yake.
Halafu Mungu hakuishia kufinyanga tu; akaendelea hatua ya mbele ya kupulizia pumzi yake ambayo ilimfanya mtu kuwa nafsi hai. Hili sio jambo la kawaida. Yaani uhai wa mwanadamu unagharimu pumzi ya Mungu mwenyewe, na sio hewa ya oksijeni tu.
Sasa kama unadhani ni jambo la kawaida, embu mfuate mfinyanzi yeyote au mchonga vinyago akiwa na vinyago vyake halafu mwambie aipulizie pumzi yake uone kama vinyago vitakuwa nafsi hai.
Hapo ndipo utakapokubali kuwa, uumbaji wa mwanadamu alioufanya Mungu ni ajabu.
(ii) Mtu Kutoka Ubavu wa Mwanadamu (Mwanzo 2:21-23)
“BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa kmaana ametwaliwa katika mwanamume.”
Hii ni ajabu nyingine; ya kwamba ubavu (tena mmoja) umetumiwa na Mungu kumfanya kiumbe kingine, mwanamke. Unaweza kujiuliza, imekuwaje Uumbaji uliomgharimu Mungu kutumia mavumbi ya ardhi kufinyanga na kupuliza pumzi yake, eti sasa hivi huo huo uumbaji ukamilishwe kwa kutumia ubavu mmoja tu?
Tena, uumbaji wa kiumbe jinsia ya kike. Hapo ndipo utagundua kumbe kwenye ubavu mmoja kulikua na ngozi laini, viungo vya uzazi vya mawanamke yaani mirija ya falopia, yuterasi, mji wa mimba, maumbile ya kifuani ya mwanamke, hadi sauti nyororo nyembamba.
Sasa kama unadhani ni jambo la kawaida, nenda chukua mbavu za mbuzi halafu utengeneza mbuzi mwingine tuone! Halafu chukua mbavu za mbuzi wa kiume halafu utengeneze mbuzi mwingine wa kike tuone! Ndipo utagundua kwamba, Uumbaji wa mtu kutokea kwenye ubavu mmoja wa mtu mwingine ni ajabu; sio suala la kawaida. Ni ajabu!
(iii) Mwanadamu Kuzaliwa kwa Neno (1Petro 1:23)
“kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.”
Andiko hili linaonyesha wale waliozaliwa mara ya pili (yaani wanaomwamini Kristo, waliookoka) ndio waliozaliwa kwa neno la Mungu. Hawa wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu na sio mapenzi ya mtu wala mapenzi ya mwili. Maana yake wamezaliwa kwa Mungu mwenyewe kutaka wazaliwe na sio kwa maamuzi ya mwanadamu.
Hawa hawajazaliwa kama matokeo ya msukumo wa hisia za mwili bali kwa Mungu mwenyewe. Hata hivyo, unapaswa kujua kwamba hapo mwanzo, ulimwengu wote uliumbwa kwa neno la Mungu.
Yaani malighafi ya kwanza kabisa ya Uumbaji wa ulimwengu wote ni Neno la Mungu kwanza kabla ya mavumbi ya ardhi, kabla ya ubavu, kabla ya mwanadamu. (Waebrania 11:3) “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.”
Ndio maana utaona Mungu alipotaka kumwumba mwanadamu hapo mwanzo alitamka. (Mwanzo 1:26) “Mungu akasema; Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi”
Lakini baada ya uasi kuingia, dhambi iliingia na kuvuruga mpango wa Mungu. Lakini Mungu alikuwa na mpango bora zaidi kupitia Yesu Kristo; ya kwamba wale watakaomwamini moyoni na kumkiri kwa vinywa vyao (ambao wanaitwa waliozaliwa mara ya pili au waliookoka) wataitwa wana wa Mungu yaani waliozaliwa na Mungu; waliotokana na mbegu isiyoharibika ambayo ni neno la Mungu.
Kwa hiyo, unapaswa kufahamu ya kwamba malighafi ya kwanza iliyotumika kukufanya wewe na mimi sio mavumbi ya ardhi, wala sio ubavu, wala sio mbegu za baba yako na mayai ya mama yako bali ni neno la Mungu.
Vile vile malighafi inayotumika kukuzaa mara ya pili baada ya kuokoka pia ni Neno la Mungu. Neno ndio linalokutakasa. Yesu katika maombi yake kwa Mungu Baba anasema, “…uwatakasa na ile kweli. Neno lako ndio kweli.”
Kwa hiyo mimi na wewe ni matokeo ya Neno. Wewe na mimi ni NENO ALIYEFANYIKA MWILI.
Nimeandika kitabu kinachotambulisha thamani yako kwenye macho ya Kimungu, sawa sawa na vile Mungu anavyokutazama. Kinaitwa MIMI NI NENO ALIYEFANYIKA MWILI. Kama unahitaji nakala yako unaweza kuwasiliana na mwandishi kwa namba 0657342567.
Nakutakia matokeo chanya.
Leave a comment