Mungu hathamini tu kile tunachotoa, bali moyo na imani iliyopo nyuma ya kile tunachotoa. Watu wengi hutoa kwa sababu ya desturi, hofu, au shinikizo, lakini sadaka inayogusa moyo wa Mungu ni ile inayotolewa kwa imani na furaha.
2 Wakorintho 9:7 (SUV)
Kila mmoja na atoe kama alivyokusudia moyoni mwake; si kwa huzuni, wala si kwa kulazimishwa; kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa furaha.
Najua kuna fundisho la Mungu anataka umtole sadaka ile ambayo moyo wako utauma na pengine umekuwa ukiamini hivyo lakini hiyo siyo sadaka ambayo Mungu anaipenda. Andiko letu la msingi limetaja “Si kwa huzuni” kwenye tafsi ya andiko kutoka Kigiriki limetumika neno “lupē” likimaanisha “huzuni, uchungu au majuto” sadaka ambayo inaleta vitu hivi haimpendezi Mungu.
Kutoa kwa imani ni kusema, “Ninaweza kuwa na kidogo/kikubwa lakini ninamwamini Mungu kama mtoaji wangu.” Ni kutangaza kwa vitendo kwamba Mungu ndiye chanzo cha kila kitu ulichonacho, na kwamba unamtegemea Yeye zaidi ya mali zako.
Katika agano jipya, utoaji sio sheria bali ni tunda la upendo, imani, na ufunuo. Tunapotoa kwa moyo wa shukrani, tunashirikiana na Mungu katika kazi zake, na tunajiwekea hazina ya kiroho na kimwili.
Shallom!
MAANDIKO YA ZIADA;Mithali 3:9-10, Kumbukumbu la Torati 15:10, Mithali 11:24-25, Luka 6:38.
TONO LA DHAHABU.
“Utoaji wa kweli huanzia moyoni, ukiongozwa na imani. Mungu anatamani ukue katika utoaji na utoe katika roho na kweli kwa moyo wa furaha na shukrani.”
OMBA NAMI;
Baba, ninakushukuru kwa kuniwezesha kuwa mshirika katika kazi zako kupitia kile ulichoweka mikononi mwangu. Nifundishe kutoa kwa moyo wa imani na furaha, nikijua kuwa Wewe ni mtoaji mkuu. Ninatangaza kuwa siishi kwa kutegemea kile nilicho nacho, bali kwa kutegemea neema yako isiyo na kipimo. Katika jina la Yesu, Amina.
Leave a comment