Home Biblical Manhood - Men of Faith & Responsibility Hiki Ndicho Wakifanyacho Wanaume Kudhani Wanatibu Majeraha na Maumivu Yao na Kujilinda
Biblical Manhood - Men of Faith & ResponsibilitySwahili Articles

Hiki Ndicho Wakifanyacho Wanaume Kudhani Wanatibu Majeraha na Maumivu Yao na Kujilinda

Share
Hiki Ndicho Wakifanyacho Wanaume Kudhani Wanatibu Majeraha na Maumivu Yao na Kujilinda
Share

1. KUKAA KIMYA

Wanaume wengi hawaongei yanayowasibu kwa kuogopa kuonekana dhaifu. Kwa hiyo wanabaki na maumivu ya ndani kwa ndani.

Ukimya wao unawafanya waonekane wako sawa na hakuna changamoto inayowasibu. Wengi wanadhani kukaa kimya ndio namna bora ya kuhimili changamoto wanazokutana nazo. Wengine ukimya unawapelekea kushindwa kufanya maamuzi yaliyotakiwa kufanywa na wao. Ukimya wao unaua mpaka uwezo wa kufanya maamuzi. Mifano:

Mzee Yakobo Baada ya Kusikia Dina, Binti yake Amebakwa – Alikaa kimya.

Hakuitisha kikao cha familia, wala kumwita Dina kuzungumza nae wala kuwaita familia ya kijana aliyembaka Dina na kumbikiri.

Familia ya Shekemu, kijana aliyembaka na kumbikiri Dina ilipokuja kuonana nae ili kufanya mapatano; yeye Yakobo bado hakuzungumza chochote wala kufanya maamuzi. Badala yake wanae wa kiume ndio walikuwa wakifanya maamuzi huku yeye akiwa kimya.

Hatimaye tunagundua kumbe alikuwa kimya kwa sababu aliogopa kuangamizwa endapo angefanya maamuzi yaliyotakiwa kufanyika. Maana anasema ” …kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu.” (Mwanzo 34:30)

Kwa upande mwingine aliogopa endapo angeruhusu msamaha basi wanae na familia nzima ingemchukulia kama msaliti wa familia na mtu asiyejali familia. Maana alipoulizwa na wanawe, “…Je! Ni vema amtendee umbu letu kama kahaba?” Yakobo hakuweza kujibu lolote. Hii inaonyesha hofu ya kuonekana baba asiyejali. Kwa hiyo suluhisho alilofikiri ni kukaa kimya ili kujiepusha na hukumu kama matokeo ambayo yangetokea kwa yeye kuzungumza na kufanya maamuzi juu ya jambo lile gumu la kifamilia.

Absalomu baada ya kusikia Tamari, dada yake amebakwa na Amnoni, kaka yao.

Ndugu watatu; Absalomu, Tamari na Amnoni ambao ni wana wa Daudi wanaingia kwenye mgogoro mkubwa unaopelekea visasi.

Tamari na Absalomu ni ndugu wa tumbo moja, yaani wanatoka kwa mama mmoja. Wote kaka yao ni Amnoni kwa sababu baba yao ni mmoja, mfalme Daudi.

Amnoni anamtamani kingono Tamari, dada yake na anapanga njama mpaka anafanikiwa kumbaka na baada ya kumbaka akamfukuza kwa chuki.

Absalomu aliposikia habari hiyo akakaa kimya. Akamwambia Tamari dada yake, “…je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili…” (2Samweli 13:20)

Ni kama anatoa ushauri na faraja kwa dada yake kwamba asilitie moyoni jambo hilo kumbe yeye mwenyewe amelitia moyoni jambo hilo kwa miaka miwili.

Absalomu hakuzungumza. Hakutaka kikao na nduguye Amnoni ili wayazungumze yaishe. Wala baba yao, mfalme Daudi haionekani anawaita kuwapatanisha na kuwazungumzisha ili kusuluhisha. Zaidi sana anaonekana “kukasirika sana” halafu hakuna hatua anayoichukua.

Kwa hiyo familia ya kifalme ikawa inaishi kwa kunafikiana kwa sababu ha ukimya wa wanaume wa familia hiyo kwa miaka miwili. Inaelezwa kwamba “…Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.” (2Samweli 13:22)

Baada ya miaka miwili kupita, Absalomu anapanga njama ya kulipiza kisasi na anafanikiwa kumwua Amnoni, kaka yake. Na baadaye kupanga kumpindua baba yake ili kushika nafasi ya kuwa mfalme wa Israeli.

Haya yote ni matokeo ya mwaume kukaa kimya.

2. KUNYAMAZISHA WENGINE

Mbali na kuwa na uwezo wa kunyamaza, wanaume pia wanauwezo wa kunyamazisha wengine.

Endapo mwanaume atahisi kwamba uanaume wake uko hatarini, kwa kudharaulika na kuaibishwa basi anakuwa tayari kujilinda kwa gharama yeyote hata kama gharama hiyo inamaanisha “kunyamazisha wengine”

Kikawaida anapotokea mtu au kundi la watu linalofunua udhaifu wa mwanaume au kuonekana kutishia heshima na hali ya ushawishi ya mwanaume basi kuna wanaume watakuwa tayari kunyamazisha hayo makundi ya watu au huyo mtu.

Wanaweza kunyamazisha kwa kutoa vitisho, kuongeza ubabe, kuwa watu katili, kuteka hata kuua. Kuna wanaume wengi wamenyamazisha wake zao, wazazi wao, watoto wao, familia zao na hata watu wanaowaongoza huko kazini ili kujilinda kuonekana dhaifu.

Wanahakikisha udhaifu wao unakua siri na hauzungumzwi na yeyote. Wanadhani njia mojawapo ya wao kuheshimiwa na kuwa na ushawishi ni kwa kuzuia watu wasijue kuhusu udhaifu wao hata kama watu hao wana lengo jema la kuwasaidia.

Kwenye familia utakuta mke na watoto wanajua kwamba baba anakosea lakini hawawezi kushauri vinginevyo kwa sababu wamenyamazishwa kwa vitisho au ubabe wa baba wa hiyo familia.

Kwenye kazi unakuta wafanyakazi hawawezi kushauri mambo ya kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi kwa sababu kufanya hivyo kunatishia “heshima na ushawishi” wa bosi. Kuna wanaume viongozi wa taasisi ambao ukiwapinga au kuwa na mawazo tofauti na mawazo yao au ukawa na ushawishi zaidi yao basi unapewa barua ya kuhamishwa au kusimamishwa kazi kama njia ya kunyamazishwa. Mifano:

Kaini Kumnyamazisha Habili

“Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani].

Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.” (Mwanzo 4:8)

Kaini aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Adamu alimnyamazisha ndugu yake Habili kwa sababu sadaka yake haikukubaliwa na Mungu ila sadaka ya Habili nduguye ilikubaliwa.

Kukubaliwa kwa sadaka ya Habili na kukatakiwa kwa sadaka ya Kaini kulikuwa kunatishia hadhi ya Kaini kama mzaliwa wa kwanza. Kaini alidhani heshima yake na ushawishi wake kwa ndugu yake Habili utapungua na atashindwa kutawala kama anavyotaka. Hivyo, suluhisho alilofikiri ni kumwua Habili nduguye kama njia ya kumnyamazisha.

Ubaya ni kwamba kwenye kila tukio la kunyamazisha wengine kunazaliwa tukio lingine la kunyamaza, yaani kutokusema uliyoyatenda kunyamazisha wengine.

Kaini anaficha aliyoyatenda kwa Habili baada ya Mungu kumwuliza, “…Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwanzo 4:9)

Kaka zake Yusufu kumnyamazisha Yusufu, ndugu yao, bwana ndoto.

Wana wa Yakobo waliona ndoto za ndugu yao Yusufu zinahatarisha “heshima na ushawishi” wao na kama wangeendelea kuzisikia hiyo ingemaanisha wangezidi kukosa kibali machoni pa baba yao na jamii yao.

Wakaambizana, “…Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.” (Mwanzo 37:19-20)

Nia yao ilikua kumwua ili kumnyamazisha na kuzinyamazisha ndoto zake. Lakini kuna ndugu yao mmoja, Reubeni aliwaambia wasimuue badala yake wamtupe kwenye birika lisilokuwa na maji.

Hata hivyo baadaye walimzunguka Reubeni na wakamwuza Yusufu kama mtumwa kwa wafanyabiashara Wamidiani wakaondoka naye kwenda Misri.

Baadae Reubeni anachungulia kwenye birika hamwoni Yusufu na anaanza kutaabika na kusema, “…Mtoto hayuko, nami niende wapi?” (Mwanzo 37:30)

maana walinyamaza kimya wasimwambia Reubeni walichokifanya dhidi ya ndugu yao Yusufu na wote wakaongozana kwenda kumdanganya baba yao kwamba Yusufu ameraruliwa na mnyama mkali.

Juhudi za Herode Kumnyamazisha Yesu, Mfalme wa Wayahudi.

Mamajusi wa mashariki walipokwenda kwa mfalme Herode kumwuliza, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” (Mwanzo 2:2)

Mfalme Herode akakasirika. Akajua kwamba nafasi yake kama mfalme iko hatarini. Hivyo akawatuma kijanja hao mamajusi kujua alipozaliwa huyo mtoto Yesu, mfalme wa Wayahudi ili aende kumwua.

Lakini mamajusi walizuiwa kurudi kwa Herode na hivyo Herode akatoa amri ya kwamba wauawe watoto wa kiume chini ya miaka miwili ili kumnyamazisha mfalme aliyezaliwa. (Mathayo 2:16)

3. KUTOROKA

Wanaume wengi wanadhani njia mojawapo ya kuepuka maumivu yao ni kwa kukimbia – KUTOROKA. Kuna waliotoroka kwa hofu ya kukabiliana na majukumu yaliyowekwa mbele yao kama Yona. Kuna waliotoroka kwa hofu ya kuhukumiwa kama Absalomu. Na kuna waliotoroka kwa sababu wanadhani ndio njia pekee watapata pumziko kama Yuda Iskariote.

Kutoroka Mfano wa Yona. (Yona 1:1-3)

“Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.”

Huku ni kukimbia majukumu. Ni kutoroka kwa sababu ya uoga wa kuwajibika. Kuna wanaume wengi sana wametelekeza familia zao kwa uoga wa kubeba majukumu ya malezi na kuhudumia familia kwa mahitaji.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kenya katika wilaya ya Iringa mkoani Iringa aliwahi kusema alipokuwa kwenye mahojiana na chombo cha habari cha Mwananchi, kwamba, ” Kesi nyingi nimezipata kuhusu wanaume kukimbia familia zao, nimezifikisha ofisi ya kijiji, tukawatafuta lakini hatujawapata.”

Huku mwenyekiti wa kijiji cha mtera katika wilaya ya Iringa mkoani Iringa naye alisema, “…kuna wakati wanawake wanakuja ofisini wakilalamika watoto wameshindwa kwenda shule kwa sababu hawana vifaa. Kwa hiyo sisi tunachukua jukumu la kuwatafuta waliko waume zao…”

Alieleza pia kwamba, kwa mwaka hupokea wastani wa kesi tano za wanawake wanaofika kudai talaka kutokana na waume zao kuwakimbia na kushindwa kumudu mahitaji ya familia. Wanaume wengine huzima simu ili kutopatikana kabisa.

Hali hii imeenea nchi nzima na duniani kote na kusababisha familia nyingi kulelewa bila uwepo wa baba.

Kutoroka Mfano wa Absalomu (2 Samweli 13:28-30,34)

“Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia. Lakini Absalomu akakimbia…”

Huku ni kutoroka kwa kuogopa kuhukumiwa. Kuogopa adhabu kali ambayo iko mbele yako kukukabili.

Kuna wanaume wengi sana ambao kwa makosa yao wenyewe wameshindwa kuwa jasiri na kukabili matokeo ya makosa yao na kukubali adhabu au kuomba msamaha badala yake wamechagua kukimbia – KUTOTOKA.

Kuna ambao wamewapa mabinti wadogo walio wanafunzi ujauzito na wakatoroka. Kuna ambao wamefanya ubadhirifu na wizi wa fedha kwenye ofisi zao na baada ya kugundulika wakatoroka.

Kutoroka Mfano wa Yuda Iskariote (Mathayo 27:3-5)

“Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.”

Juni 8, 2022 Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam ACP Muliro Jumanne Muliro alitoa ripoti kuhusu tukio la mwanaume aliyekuwa na miaka 34 mkazi wa Temeke kumwua aliyekuwa mpenizi wake mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Mbagala kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni; na baadaye kijana huyo wa kiume kunywa sumu na kujiua. Chanzo cha mauaji hayo hakijulikani. (Gazeti la The Citizen, 2022)

Huku ni kutoroka kwa kudhani unatafita pumziko la milele mbali na maumivu ya moyo. Wanaume wengi wamedhani kuwa njia pekee ya kuwapa tulizo la milele ni kwa kujiua.

Wengine wanadhani kujiua ni njia ya kuacha ujumbe mzito kwa wapendwa wao ili waone jinsi gani walivyokuwa “SERIOUS” kwenye kuomba msamaha au kwenye kujutia walichokifanya au kwenye kuwapenda waliowakataa.

Nimeandika kitabu ambacho kinawanusuru wanaume kutoka kwenye mtego wa kuumia na kuwa wahanga wa majeraha ambayo yanasababishwa na wao wenyewe. Kinaitwa UANAUME WAKO USIWE TESO LAKO. Utakipata kwa kuwasiiana na mwandishi kwa namba za simu 0623342567.

Nakutakia matokeo chanya.

Share

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles
Nguvu ya Neno la Mungu
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Nguvu ya Neno la Mungu

Andiko:“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu kwa hekima yote…”...

Uwepo wa Mungu
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Uwepo wa Mungu

Katika safari yao kuelekea Kanaani, Musa hakutamani tu kufika kwenye nchi ya...

Kutoa kwa Imani na Moyo wa Furaha
Devotionals & EncouragementFinance & Stewardship in God’s WaySwahili Articles

Kutoa kwa Imani na Moyo wa Furaha

Mungu hathamini tu kile tunachotoa, bali moyo na imani iliyopo nyuma ya...

Ufalme Wake Kwanza
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Ufalme Wake Kwanza

Mathayo 6:33 (SUV): Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake;...