Kuna watu wanaona haya kupiga magoti kuomba lakini hawaoni haya kupiga simu kuombaomba msaada kwa watu. Ni bora kuwa na aibu kuombaomba kuliko kuwa na aibu kuomba kwa Mungu.
Ni rahisi kumtegemea mtu ambaye umezoea huwa anakupa kila unachohitaji kiasi kwamba ukajikuta umejijengea tabia ya kuomba-omba.
Hata kama hao watu ambao umezoea kupokea msaada kutoka kwao wameletwa na Mungu kukusaidia, unapaswa kuwa na hekima – hekima ya kuchora mpaka, na kujiambia ukweli kwamba:
“pamoja na kwamba wanaweza kunisadia kwenye kila kitu ninachohitaji, bado sitawaruhusu wawe msaada wangu kwenye kila kitu. Nitawanyimia fursa ya kunisaidia mengine ambayo ninayahitaji sana ili nijifunze kumtegemea Mungu.”
Unapowanyimia watu fursa ya kuwa msaada kwako, unafungulia fursa kwa Mungu kuwa msaada wako. Unapowafanya watu kuwa msaada wako, unamnyimia Mungu fursa ya kuwa msaada wako.
Kuna watu wakipata sehemu inayowapa msaada kila wanapohitaji huwa wana tabia ya kuegemea hiyo sehemu na kuiendea kwa kila hitaji walilonalo. Utegemezi wao ni pale walipozoelea kupokea msaada. Watapiga simu kuomba fedha, kuomba kodi, kuomba chakula, kuomba ada, kuomba mtaji, kuomba mavazi na kila kitu wanachohitaji.
Itafika wakati watadhani hawana haja ya kupiga magoti kumwomba Mungu wakati wanaweza kupiga simu kwa mtu fulani na kuomba msaada.
Ezra hakuruhusu iwe hivyo kwake. Pamoja na kwamba alikuwa ana uwezo wa kumwomba mfalme Artashasta msaada wa kikosi cha askari na wapanda farasi wa kuwalinda wakiwa njiani LAKINI bado alijua nafasi ya Mungu kama msaada pekee. Na hivyo, aliweza kujinyenyekesha na kuwaongoza wana wa Israeli kufunga na kuomba kwa ajili ya kusafiri njiani kwa amani – waliomba msaada kutoka kwa Mungu.
Unapofadhiliwa na mfalme, usijisahau ukaonyesha utegemezi wako kwake. Badala yake, onyesha utegemezi wako kwa Mungu, aliye Mfalme wa wafalme.
Badala ya kuchagua kuombaomba kikosi cha askari kutoka kwa mfalme, walichagua kuomba amani kutoka kwa Mfalme wa Wafalme.
Badala ya kuomba uwezo wa kutibiwa na matatibu mahiri wa China na India, unapaswa kupiga magoti na kuomba uponyaji na afya ya Kiungu kutoka kwa Tabibu wa ajabu.
Badala ya kupiga simu kwa mjomba aliyeko wizarani ili akupe mchongo wa ajira upate hela ya kujikimu kimaisha, unapaswa kupiga magoti na kuomba mkate wa kila siku kutoka kwa BWANA aliye Mchungaji wako.
Leave a comment