Zaburi 37:5 (SUV): Mkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.
Katika safari ya imani, kuna hatua muhimu mbili ambazo huleta matokeo ya kiungu: kumkabidhi Bwana njia yako, na kumtumaini. Kumkabidhi ni kusema, “Bwana, hii nalo ni lakwako.” Lakini kumtumaini ni kusema, “Najua hata hili utalifanya tena”
Wengi huanza vizuri wanamkabidhi Mungu maisha, mipango, au maamuzi lakini wanapokumbana na hali ngumu/changamoto, huanza kuyachukua tena mikononi mwao na kuzitegea akili na uwezo wao wenyewe. Hapa ndipo wengi hushindwa kuona kile Biblia imesema kwenye andiko letu la msingi “naye atafanya.”
Kuamini ni kujua kwamba hata usipoyaona matokeo sasa, Mungu yupo kazini. Ni imani kwamba njia Yake ni bora kuliko zako, na wakati Wake ni kamili. Wakati unamwamini Mungu kwa moyo wote, unaacha kulazimisha mambo na kuanza kuamini katika ahadi na utendaji wake.
Usichoke kusubiri, usichoke kuamini, Usirudi nyuma. Alikupa ahadi, na Yeye si mwanadamu aseme uongo. Akisema atafanya amini atafanya.
SOMO LA ZIADA: Mithali 3:5-6; Isaya 26:3
TONO LA DHAHABU:
Kumkabidhi Mungu njia zako ni mwanzo wa uaminifu; lakini kumtumaini kwa moyo wote ndiko kunafungua mlango wa matendo Yake ya ajabu.
OMBA NAMI;
Bwana, ninakabidhi njia zangu mikononi Mwako. Najua una mpango mkuu juu ya maisha yangu. Nisaidie kukuamini hata katika hali zisizoeleweka/elezeka. Najua hutachelewa, na kila ulichosema kitakuwa, kwa jina la Yesu, Amen.
Leave a comment