Home Biblical Manhood - Men of Faith & Responsibility Hivi Unajua Majukumu ya Kuwa Baba Katika Kuchunga Ujauzito?
Biblical Manhood - Men of Faith & ResponsibilityBiblical Marriage, Parenting & Family LifeSwahili Articles

Hivi Unajua Majukumu ya Kuwa Baba Katika Kuchunga Ujauzito?

Share
Hivi Unajua Majukumu ya Kuwa Baba Katika Kuchunga Ujauzito?
Share

Haipingiki kwamba Mungu alivyomwumba mwanamke alimwumba hivyo na kumfanya atofautiane kimaumbile na mwanaume kwa kusudi la kubeba kazi ya uumbaji wa Mungu ambayo ni endelevu.

Kazi hiyo ni ujauzito. Kwa hiyo wote tunaelewa vizuri kwamba ni jukumu la msingi la mwanamke kubeba na kulea ujauzito kwa kuwa yeye ndiye aliyeumbwa akiwa na mwili wenye miundombinu ya kuwezesha kazi hii ya kubeba na kulea ujauzito.

Hata hivyo, hii kazi haipaswi kuwa mzigo wake peke yake! Baba wa mtoto naye ana wajibu wa kufanya. Baba wa mtoto pia anao wajibu wa kulea – tena ni kulea kichungaji ujauzito wa mkewe.

TUONE KWA UCHACHE BAADHI YA MAJUKUMU YA BABA ALIYOAMINIWA NA MUNGU KUCHUNGA UJAUZITO

1. KUTAMKA MAMBO ILI YATOKEE KWA NGUVU YA NENO LA MUNGU

Hatima ya watu na mataifa zimeandikwa kwenye vitabu vya mbinguni. Mungu anajua na ameandika vitabuni. Lakini zinaweza zisitokee kama ilivyoandikwa kwako endapo hautatumia mamlaka yako ya kuvitamka, kuviita vitoke kwenye ulimwengu usioonekana na kushikika, vije kwenye ulimwengu unaoonekana na kushikika.

Mungu mwenyewe alipotaka kutokee mbingu na dunia hakuishia kuwaza na kuandika, alienda mbele kutumia mamlaka yake ya kitamka, akatamka na vitu vikawa kama alivyotamka. Na sasa anataka na sisi tutamke ili mambo yatokee kwetu, La sivyo, hayatatokea ijapokuwa yapo tayari kwenye ulimwengu wa roho.  Kama baba hapa duniani, Mungu anakutarajia utamke kuhusu mambo yafuatayo:

(a) Tamka Ujauzito Utokee

Najua unafahamu kwamba ili ujauzito utokee inakupasa kama baba upande mbegu za kiume kwa mkeo ili zikutane na mayai ya mkeo na ujauzito utokee na hatimaye watoto wazaliwe.

Vipi kama nikikwambia kwamba, mbegu ya kwanza kupanda kwa mkeo  ili ujauzito utokee sio mbegu za kiume!? Bali ni mbegu ya neno.

Tamka kila siku kwa mkeo sawa sawa na neno la Mungu kwenye kitabu cha Zaburi 128:3, “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako.”

Tamka kwamba, “mke wangu ni mzabibu uzaao. Atabeba ujauzito na kuzaa watoto wengi kama miche ya mizeituni. Katika Jina la Yesu.”

Kabla hujambebesha mkeo ujauzito kimwili, hakikisha unambebesha kiroho, kupitia mamlaka yako ya kutamka sawa sawa na neno la Mungu.

(b) Tamka Uwepo wa Watoto Wako Kabla Hawajazaliwa

Baba yetu wa mbinguni anatujua kila mmoja kwa majina. Ametuandika kwenye vitabu vyake huko mbinguni kabla hata hatujazaliwa. Lakini baba wengi hapa duniani huwa wanasubiri mpaka mtoto azaliwe ndio waanze kumpa jina. Wapo wachache ambao vile vile wanasubiri mpaka mimba itungwe ndio waanze kutoa jina kwa mtoto.

Ngoja nikupe ushuhuda wa walezi wetu wa kiroho, mimi na mke wangu. Mchungaji James na mke wake Frida Kalekwa, zaidi ya miaka 15 nyuma kabla hawajafunga ndoa tayari walijua jina la mtoto wao wa kwanza, ambaye ni Joshua.

Mchungaji James Kalekwa, alimjua mwanaye Joshua tangu akiwa kidato cha pili. Alianza kutambulika na kuitwa na wanafunzi wenzake wakati huo kama “baba Joshua” huku akiwa hana hata mchumba na wala hajakutana na Frida bado.

Baada ha kufunga ndoa, miezi kadhaa ikapita, akazaliwa mtoto mwanamume ambaye jina lake tayari lilijulikana kabla hajatungwa mimba. Akapewa jina Joshua.

Siku tuliposikia ushuhuda huu, tukasukumwa na sisi kutaka kuwajua watoto wetu kwa majina. Mungu akatupa majina ya watoto wetu mapacha, Great (wa kiume) na Grateful (wa kike).

Bado hatujawalimbatia kwa mikono yetu wala kuwaona kwa macho ya damu na nyama lakini tayari wapo na tunawajua kwenye ulimwengu wa roho. Hata kwenye maombi ya watoto, huwa tunawaombea kwa kuwataja majina. Kwa kuwa wapo hakika! Tumewatamka. Tumewaita.

Nataka ukumbuke kwenye sura ya kwanza tumeona kwamba, hao watoto kuwa wako sio wako tu; kwanza, ni wa BWANA kabla hujakabidhiwa wawe wako. Kwa hiyo, BWANA anawajua. Kazi yako ni kumwuliza BWANA, naye atakwambia ni akina nani na atakupa na majina yao.

Yesu alipewa jina kabla mimba haijatungwa. Malaika anawatokea Yusufu na Mariamu kwa nyakati tofauti na kuwaambia mtamwita jina lake Yesu. Na ndivyo walivyomwita.

Umuhimu wa kujua uwepo wa mwanao na jina lake ni kwamba; unapata kujua kusudi la uwepo wa mwanao na mara zote jina huwa linaelezea kusudi la mtu. Ili adui asimwite jina tofauti na kumpa jukumu tofauti na lile ambalo limefanya azaliwe hapa duniani.

(c) Tamka na tangaza baraka kwa mwanao kabla hajazaliwa:

Mungu anatamka baraka kwa Yesu kabla hata hajatungwa mimba. Malaika anamwambia Mariamu, “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:32-33. SUV)

Nataka uone hapo hizo baraka, kwamba “atakuwa mkuu”, “atamiliki nyumba ya Yakobo”. Hizi ni baraka ambazo zinatamkwa kabla hata mimba haijatungwa kumhusu mtoto Yesu.

Mungu baada ya kumwumba mtu duniani hapo mwanzo, kwa neno lake, moja ya kitu cha kwanza alichofanya ni kutamka baraka; “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:28. SUV)

Hivyo, ukiwa kama baba hapa duniani unapaswa kutamka baraka ya uzao, baraka ya maongezeko na mazidisho, baraka ya utele, baraka utawala na baraka ya umiliki kwa mwanao kabla hata hajazaliwa; na hata kabla hajawa tumboni mwa mama yake. Kuna majukumu mengi ambayo Mungu anamtarajia baba kuhusika nayo kikamilifu katika kulea ujauzito. Mengine yanapatikana kwenye kitabu cha NAFASI YA BABA KATIKA KULEA UJAUZITO. Wasiliana na mwandishi kupata nakala yako kwa kupitia namba za simu 0623342567.

Nakutakia matokeo chanya.

Share

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles
Nguvu ya Neno la Mungu
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Nguvu ya Neno la Mungu

Andiko:“Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu kwa hekima yote…”...

Uwepo wa Mungu
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Uwepo wa Mungu

Katika safari yao kuelekea Kanaani, Musa hakutamani tu kufika kwenye nchi ya...

Kutoa kwa Imani na Moyo wa Furaha
Devotionals & EncouragementFinance & Stewardship in God’s WaySwahili Articles

Kutoa kwa Imani na Moyo wa Furaha

Mungu hathamini tu kile tunachotoa, bali moyo na imani iliyopo nyuma ya...

Ufalme Wake Kwanza
Devotionals & EncouragementSwahili Articles

Ufalme Wake Kwanza

Mathayo 6:33 (SUV): Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake;...