Kuna Gharama ya Kukaa Kikao na Wafalme.
Sio rahisi kutaka kikao na wafalme. Kuna gharama kubwa ya kulipa ukitaka kufanya kikao na wafalme – wa ulimwengu huu wa mwili na hata wa ulimwengu wa roho!
Kuwa na cheo au nafasi adhimu haiondoi ukweli kwamba bado hata wewe unahitaji kulipa gharama kukaa kikao na wafalme. Cheo chako sio kigezo kinachokuepusha kulipa gharama.
Esta, pamoja na kwamba alikuwa malkia bado alihitaji kulipa gharama ili kuonana na wafalme na kufanya nao kikao.
(i) Gharama ya kuhatarisha maisha yake kwa kwenda kinyume na sheria.
Esta 4:11
Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini.
Sheria ni kwamba kama hujaitwa na mfalme halafu ukajipeleka basi unatakiwa kuuawa. Hii ni sheria ya mfalme Ahasuero. Ukitaka kuonana naye ni mpaka akuite. Huruhusiwi kujipeleka!
Ukienda bila yeye kukuita sharti uuawe.
Watu wote walijua hivyo, watumwa walijua hivyo, watu wa majimbo ya mfalme walijua hivyo, wanaume wote walijua hivyo, wanawake wote walijua hivyo, na Esta alijua hivyo.
Lakini pamoja na kuwa na ufahamu huu bado alikuwa tayari kwenda kwa mfalme bila kuitwa. Alijua fika hatari ambayo ingempata lakini bado alidhamiria kwenda, mpaka anasema, “…nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.”
Ingekuwa rahisi kwake kuogopa kwenda kwa mfalme na kukaa kusubiri huruma za mfalme huenda ataitwa na mfalme. Ingekuwa rahisi kwake kubaki na kisingizio kwamba haiwezekani, sheria haimruhusu.
Lakini alikubali kuingia gharama. Gharama ya kuweka maisha yake rehani kwa ajili ya hatima yake na watu wake.
Kulipa gharama ni kutoruhusu kisingizio chochote kile kikuzuie kufanya unachotakiwa kufanya au kupata unachotakiwa kupata
(ii) Gharama ya Kuwa Kuhani kwa Ajili ya Watu Wake.
Kuwa kuhani ni namna nyingine ya kwenda kinyume na sheria.
Kikawaida mtu haanzi kwenda kwa bosi mkubwa kutaka haki kabla ya kupita kwa bosi chini yake. Kikawaida mtu haruhusiwi kuruka mamlaka iliyo juu yake ili kwenda kwenye mamlaka ya juu zaidi ya ile iliyo juu yake.
Kikawaida hii ni utovu wa nidhamu. Ni uasi. Ni kusema huna imani na kiongozi aliye juu yako na ndio maana umeenda kwanza kwa aliye juu yake!
Kikawaida Esta alipaswa kusubiri mpaka apate nafasi ya kuonana na mfalme Ahasuero na sio kwenda kwa mwenye mamlaka ya juu zaidi yake.
Lakini bado Esta alikwenda kinyume na ukawaida, alikwenda kinyume na utaratibu. Alianza kufanya kikao na mwenye mamlaka ya juu zaidi ya kiongozi aliye juu yake. Alianzia kwanza kufanya kikao na Mfalme wa wafalme.
Kwenye ulimwengu huu wa mwili hii inatafsiriwa kama utovu wa nidhamu na uasi lakini kwenye ulimwengu wa roho inatafsiriwa kama ukuhani.
Ukuhani ambao hata hivyo sio jukumu jepesi. Ni jukumu ambalo linamtaka Esta asimame mbele ya Mfalme kwa ajili ya watu wake. Utakumbuka namna makuhani walipotaka kwenda mbele za Mungu kwa ajili ya watu wake ilibidi ajitakase maana akiingia mahali patakatifu pa patakatifu na hatia yeyote ile atakufa hakika.
Ilimgharimu kufunga na kuomba kuingia kwa mfalme Ahasuero na apate kibali asiuawe. Vile vile ilimgharimu kufunga na kuomba kutoshea kukaa kikao na Mfalme wa wafalme ambaye huwa hakai kikao na wenye mwili.
(iii) Gharama ya Kufunga na Kuomba
Suala la kufunga na kuomba ni gharama. Ni gharama ya kuacha chakula na kunidhamisha mwili kuomba. Gharama hii ni kubwa kwa Esta, ambaye ni malkia. Malkia amezungukwa na starehe zote anazohitaji lakini bado aliacha vyote ili kufunga na kuomba.
Alitambua kuwa pamoja na kwamba mwili wake unahitaji chakula lakini kuna kitu anachokihitaji zaidi ya chakula. Alitambua kuwa pamoja na kwamba nafsi yake ingependa kuburudika na viburudisho vya kila aina kwenye jumba la kifalme lakini kuna kitu nafsi yake inakihitaji zaidi ya burudiko la muda mfupi. Alitambua kwamba anahitaji kupata uhuru dhidi ya hukumu ya kifo iliyotangazwa kwa watu wake.
Na kama gharama ya kupata uhuru huo ni kufunga na kuomba, basi alikuwa tayari kuilipa na alilipa gharama hiyo.
Tena ukumbuke ya kwamba Esta alikuwa malkia kwenye taifa lisilo lake. Kwenye taifa ambalo haliamini anachokiamini wala haliabudu anachoabudu! Taifa linaloabudu miungu yao ya sanamu.
Lakini utaona Esta anapata ujasiri wa kutoa amri mpaka kwa vijakazi wake wafunge na kuomba kwa Mungu wa wayahudi, ambaye hakuwa Mungu wa waajemi – jambo ambalo ni hatari sana kufanywa na malkia ndani ya himaya ya mfalme ambaye yupo kinyume na Mungu wa wayahudi.
Kuna kitabu kizuri kinaitwa WANACHOKIFANYA MALKIA KUPATA WANACHOKITAKA ambacho kitakupa akili ya kuwashawishi wafalme kukupatia kile unachokitaka. Kinapatikana kwa kuwasiliana na mwandishi kwa namba za simu 0623342567.
Nakutakia matokeo chanya.
Leave a comment