Mara nyingi Mungu akitaka kuwakomboa watu wake huwa anatumia mbinu inayoonekana kana kwamba anaruhusu watu wake wapigwe, waumizwe na kuangamizwa. Lakini katika huko kupigwa, huko kuumizwa na kuonekana kwamba wanaangamizwa ndiko anakojipatia ushindi na kuwapatia watu wake ukombozi.
Taswira ya kushinda kwenye fikra na macho ya Mungu inaweza kuonekana ni taswira ya kushindwa kwenye fikra na macho ya kibinadamu. Angalia mifano hii:
1. Kifo cha Yesu ndio Ukombozi wa Ulimwengu
Mungu anatoa ahadi ya ukombozi wa wanadamu hapo mwanzo kwenye bustani; anasema uzao wa mwanamke utamponda nyoka kichwa na nyoka atakigonga kisigino chake. (Rejea Mwanzo 3:15)
Hii ni kumaanisha kwamba, kwenye taswira ya kibinadamu utaona nyoka anafukuzia kisigino cha uzao wa mwanamke ili akigonge na anakignga kweli. Na sumu inaathiri kisigino na huyu mtu aliyegongwa na nyoka ataonekana kana kwamba ameopoteza maisha. Lakini vile vile, wakati nyoka anagonga kisigino, yeye hapo hapo anapondwa kichwa na kufa.
Ndicho alichokifanya BWANA Yesu msalabani. Shetani na mawakala wake walidhani wamemwangamiza mfalme wa Wayahudi kumbe kupitia huo msalaba, ndivyo ulimwengu ulivyookolewa na Yesu akamnyang’anya shetani funguo za mamlaka alizoiba kipindi cha Adamu na Hawa pale bustanini.
2. Kuuzwa, Kusingiziwa na Kufungwa Jela kwa Yusufu ndio Ukombozi wa Watu wa Misri na Mataifa Jirani.
Yusufu aliuzwa na ndugu zake kuwa mtumwa, akasingiziwa amebaka mke wa bosi wake Potifa, akahukumiwa kifungo jela. Akiwa jela akatafsiri ndoto za wajakazi wawili wa Farao na zikatimia.
Farao akaota ndoto iliyowashinda wataalamu na wachawi wa Misri yote kutafsiri. Akaitwa Yusufu aliyewatafsiria ndoto wajakazi wa Farao. Yusufu akatafsiri na kutoa ushauri wa nini kifanyike. Farao akampa cheo na mamlaka juu ya nch yote ya Misri. Akawaokoa Wamisri na watu wa mataifa mengine kutoka kwenye baa la njaa.
Kati ya watu waliookolewa ni ndugu zake ambao walimwuza. Baada ya kukutana nao na kuwafadhili anawaambia; “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.” (Rejea Mwanzo 50:20)
Penye Nyuki Pana Asali
Kwa hiyo, ni kama Mungu anaruhusu nyuki wakung’ate, upate maumivu yatakayokufanya utoe machozi halafu katika huko kung’atwa na nyuki uweze kupata faida mara mbili: (1) faida ya kuimarishwa kinga ya mwili kwa sumu ya nyuki (2) kufaidi asali ya nyuki.
Hii ni sawa na kitendawii ambacho Samsoni aliwapa Wafilisti wakashindwa kukitegua; “…Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu…” (Waamuzi 14:14)
Kwa mwenye kula hatutarajii kitoke chakula bali tunatarajia chakula kiliwe kiishe na kisiwepo. Lakini Mungu anakusudia kwa huyo mwenye kula kitoke chakula.
Kwa mwenye nguvu tunatarajia yatoke mapigo ya kuumiza na yatakayoleta uchungu. Lakini Mungu anakusudia kwa huyo mwenye nguvu, utamu utokee hapo.
Kuna nyakati za kilio kikuu ambazo wewe unadhani unalia kwa uchungu na huzuni lakini Mungu anataka kwenye nyakati hizo hizo ulie kwa furaha. Kichwani mwako na machoni pako unaona dalili zote za huzuni lakini kichwani mwa Mungu na mbele ya macho yake anaona dalili zote za furaha. Na anataka kukuonesha uwaze hivyo na uone hivyo na hatimaye ukilia, ulie kwa furaha.
Anataka kuyapa maana sahihi machozi yako. Hataki yaende bure. Lakini kuna mambo ambayo lazima ashughulike kuyandoa kwako ili yasikuzuie kuona vile unavyopaswa kuona.
Kwenye sura inayofuata tutakwenda kuona mambo ambayo yatafanya machozi yako yasiwe na maana sahihi kama ile ambayo Mungu amekusudia.
Lengo ni kwamba, Mungu anataka uone ya kwamba ni furaha tupu hata wakati wa majaribu.Ili badala ya kutoa machozi ya huzuni, uanze kutoa machozi ya furaha. Halaluya!
Kuna kitabu kizuri ambacho kitakupa hekima ya namna ya kuyapa machozi yako maana sahihi, kinaitwa MAMA, UNALILIA NINI? Utakipata kwa kuwasiliana na mwandishi moja kwa moja kwa namba ya simu 0623342567.
Nakutakia matokeo chanya.
Leave a comment