Andiko:
“Maana Bwana ni mwema; fadhili zake ni za milele, Na uaminifu wake hudumu kizazi hata kizazi.” Zaburi 100:5
TAFAKARI:
Katika dunia inayobadilika kila siku, ni baraka kubwa kujua kuwa Mungu habadiliki. Yeye ni yule yule jana, leo na hata milele. Uaminifu wake si wa msimu, si wa hali au hisia ni wa kudumu.
Wakati watu wanabadilika, ahadi zao zikivunjika, na mazingira yakionekana kutoeleweka, Bwana wetu husalia mwaminifu. Anafanya kile asemacho, na hatashindwa kutimiza ahadi zake juu ya maisha yako.
Kumbuka nyakati alizokupigania, alizokutunza, na alizojibu maombi yako. Huo ni ushahidi kuwa bado yuko kazini leo. Usiache kumtumainia. Ataendelea kuwa mwaminifu kwako na kwa kizazi chako.
TONO YA DHAHABU:
Uaminifu wa Mungu ni thabiti kama mwamba. Tazama nyuma kwa shukrani, tazama sasa kwa imani, na tazama mbele kwa tumaini.
OMBA NAMI:
Baba mwenye upendo, nakushukuru kwa uaminifu wako usio na mwisho. Nikikumbuka wema wako, najaa shukrani na tumaini. Nisaidie kukuamini hata ninapoelekea katika siku zisizojulikana, nikiwa na hakika kwamba wewe hudumu milele. Katika jina la Yesu, Amina.
BLESSED
Leave a comment