Kwenye hatari huwa tunakuwa waangalifu. Tunaongeza umakini. Huwa tunafuata mwongozo wa namna ya kuenenda kwenye hatari ili tuwe salama. Huwa kuna vifaa kinga tunavaa kujikinga kwa hizo hatari zisitudhuru bali tubaki salama.
Uwepo wa hatari hakutuzuii kufanya mambo au kuyaendea mambo. Kuwepo kwenye nyakati za hatari hakutuzuii kufanya mambo au kuayendea mambo. Kuwa mwanamke anayeishi katika nyakati za hatari hakukuzuii kuwa mama. Hatari zinazoambatana na kuwa mama hazipaswi kukufanya uogope kuchukua uamuzi wa kuwa mama.
Hata hivyo, kufahamu ya kuwa kuna hatari kunapaswa kukufanya uongeze umakinifu wako na kukupa kutaka kujua mwongozo wa kufuata ili unapoyaendea mambo kwenye hatari uyaendee kwa hekima ukiwa umejikinga ili uendelee kubaki salama.
Kuwa mama katika nyakati hizi ni jambo la hatari. Hata hivyo, sio jambo baya. Wala hautishiwi “usiwe mama”. La hasha! Bali unapewa tahadhari kusudi uwe makini sana kwenye kuendea uamuzi wa kuwa mama kibaiolojia na kimalezi kwa usalama wako na watu wengine.
Makala hii sio bango linalopiga kelele kukwambia: SIMAMA! KUWA MAMA NI HATARI. HIVYO USIWE MAMA! KAA MBALI NA KUWA MAMA! La hasha!
Bali ni bango linalokupa tahadhari kwamba: KUNA HATARI ZA KUWA MAMA. HIVYO KUWA MAKINI. FUATA MUONGOZO HUU ILI UWE MAMA USIYEDHURIKA NA HATARI. Ni ili kuhakikisha usalama wako na watu wengine.
Kwenye makala hii utapata kujua maamuzi yanayofanywa na akina mama kwenye nyakati za hatari ambayo hutafsirika kuwa maamuzi ya kishujaa yanapofanywa kwa ufahamu mzuri na yanaweza vile vile kuhatarisha maisha yanapofanywa bila ufahamu mzuri. Utagundua kuna mstari mwembamba sana unaotenganisha maamuzi ya kishujaa na maamuzi hatarishi.
TUONE MIFANO YA MAAMUZI YALIYOFANYWA NA AKINA MAMA KATIKA NYAKATI ZA HATARI

Kutoka 1:22
“Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai. “
Endelea kusoma Kutoka 2:1-10
“Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.”
Ukisoma kitabu cha Kutoka Sura ya 1 kuanzia mstari wa 8 hadi 22 utaona muktadha wa nyakati za hatari. Anaibuka Kiongozi wa Misri, Farao ambaye hamjui Yusufu na kwa hiyo hamjui Mungu wa Israeli. Anawafanya wana wa Israeli kuwa watumwa. Wana wa israeli walipokuwa wanaongezeka kiidadi akaweka amri ya kuuawa kwa watoto wa kiume wote watakaozaliwa na waebrania.
Kuna maamuzi tunaona yanafanywa na akina mama katika kipindi hicho. Moja ya hayo maamuzi ni:
Kuona ya Kwamba Amezaa Mtoto Mzuri

Kwenye nyakati za hatari ambazo watoto wanaozaliwa wa kiume wanawindwa kuuawa na Farao, bila shaka maombi ya wanawake wengi wajawazito wa Misri ni kuzaa mtoto wa kike na sio wa kiume.
Huwezi kufikiria na kudhani kwamba binti wa Lawi alikuwa anaomba kwa bidii kuzaa mtoto wa kiume. Sio kwamba hakuwa anapenda kuwa na mtoto wa kiume ila nyakati zile zilimfanya aone itakuwa bora kama akizaa wa kike ili aepuke na dhahama ya msiba wa kuomboleza mauti ya mtoto akiwa bado mchanga.
Lakini biblia inatuambia kwamba, “akazaa mwana [mtoto wa kiume], na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.” Pamoja na kwamba kuzaa mtoto wa kiume kulimaanisha kuzaa haramu kwa mujibu wa nyakati zile lakini yeye hakuona haramu. Hakuona ni mbaya. Aliona amezaa mtoto mzuri.
Kuna wanawake ambao waume zao au wakwe wameweka shinikizo kwao kuzaa mtoto wa jinsia fulani. Unakuta mwanaume na ndugu wa mume wanataka mwanamke azae mtoto wa kiume ili apatikane mrithi. Hii imewafanya wanawake wengi kuwa kwenye presha ya kuomba kuzaa mtoto mwenye jinsia fulani kulingana na matakwa ya mume au wakwe.
Ikitokea wamezaa mtoto mwenye jinsia tofauti na walivyotarajia, chuki inaamia kwa mtoto. Na ni chuki iliyoambukizwa kutoka kwa wakwe, kwenda kwa mume, kwenda kwa mama dhidi ya mtoto. Ndio maana mtu amefanikiwa kujifungua lakini akitajiwa jinsia ya mtoto, furaha yake inapungua. Anapoteza changamko. Kwa sababu hajazaa mtoto mwenye jinsia iliyotarajiwa.
Wengine wamezaa watoto wenye changamoto fulani. Na kwa sababu hawakuitarajia hiyo changamoto basi wamejikuta wana chuki dhidi ya walichokizaa.
Binti wa Lawi alikataa kuruhusu chuki ya Farao dhidi ya watoto wa kiume wa Kiebrania iambukizwe kwake. Ijapokuwa sheria ya nchi inachukia kuzaliwa mtoto wa kiume, inawezekana nyakati zile wanawake walichukia kuzaa watito wa kiume lakini yeye aliona kuwa amezaa mtoto mzuri. Hakuona kwamba amezaa haramu. Hakuona kwamba amezaa bahati mbaya! bali ni mtoto mzuri.
Inagharimu ushujaa kuona uzuri kwenye jambo linaloonekana baya na kupigwa vita vikali kwenye jamii ya watu wengi.
Matarajio ya Farao yalikuwa kwa gharama yeyote watoto wa kiume wasiishi. Kwa hiyo angependa awaue au wauawe na mama zao kwa sababu ya chuki au hofu.
Binti wa Lawi hakukubali kulisha matarajio ya Farao. Na wewe ninakuombea kwa BWANA ya kwamba hautalisha matarajio ya shetani katika jina la Yesu. Amina.
Nimeandika kitabu kinachowapa akina Mama tahadhari na kuwasaidia kufanya maamuzi ya kishujaa na kuepuka maamuzi hatarishi kwenye nyakati za hatari. Kinaitwa HATARI ZA KUWA MAMA KWENYE NYAKATI ZA HATARI. Unaweza kuwasiliana na mwandishi ukihitaji nakala yako kupitia namba 0657342567.
Nakutakia matokeo chanya.
Leave a comment